Masomo ya Misa, Jumapili ya 33, Mwaka C. 13/11/2022

Somo la Kwanza
Mal 4:1-2
Angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi.Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake;

Wimbo wa Katikati
Zab 98:5-9
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
(K) Bwana anakuja awahukumu mataifa kwa haki.

Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha mbele za Bwana;
(K) Bwana anakuja awahukumu mataifa kwa haki.

Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa adili.
(K) Bwana anakuja awahukumu mataifa kwa haki.

Somo la Pili
2The 3:7-12
Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.

Shangilio
Lk 21:36
Aleluya, aleluya
Kesheni kila wakati, mkiomba, ili mpate kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
Aleluya

Somo la Injili
Lk 21:5-19
Watu kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, alisema, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni. Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwaua magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.